Matthew 19:16-30
16Mtu mmoja alimjia Yesu, akamwuliza, “Mwalimu, nifanye kitu gani chema ili niupate uzima wa milele?”i
17Yesu akamwambia, “Mbona unaniuliza kuhusu jambo jema? Kuna mmoja tu aliye mwema. Ukitaka kuingia katika uzima, shika amri.”
18Yule mtu akamwuliza, “Amri zipi?” Yesu akasema, “Usiue, usizini, usiibe, usitoe ushahidi wa uongo,
19waheshimu baba yako na mama yako; na, mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe.”
20Huyo kijana akamwambia, “Hayo yote nimeyazingatia tangu utoto wangu; sasa nifanye nini zaidi?”
21Yesu akamwambia, “Kama unapenda kuwa mkamilifu, nenda ukauze mali yako uwape maskini hiyo fedha, nawe utakuwa na hazina mbinguni, kisha njoo unifuate.”j
22Huyo kijana aliposikia hayo, alienda zake akiwa mwenye huzuni, maana alikuwa na mali nyingi.
23Hapo Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Kweli nawaambieni, itakuwa vigumu sana kwa tajiri kuingia katika Ufalme wa mbinguni.k
24Tena nawaambieni, ni rahisi zaidi kwa ngamia kupita katika tundu la sindano, kuliko kwa tajiri kuingia katika Ufalme wa mbinguni.”l
25Wale wanafunzi waliposikia hivyo walishangaa, wakamwuliza, “Ni nani basi, awezaye kuokoka?”
26Yesu akawatazama, akasema, “Kwa binadamu jambo hili haliwezekani, lakini kwa Mungu mambo yote huwezekana.”m
27Kisha Petro akasema, “Na sisi je? Tumeacha yote tukakufuata; tutapata nini basi?”n
28Yesu akawaambia, “Nawaambieni kweli, Mwana wa Mtu atakapoketi katika kiti cha enzi cha utukufu wake katika ulimwengu mpya, ninyi mlionifuata mtaketi katika viti kumi na viwili mkiyahukumu makabila kumi na mawili ya Israeli.o
29Na kila aliyeacha nyumba, au ndugu, au dada, au baba, au mama, au watoto, au mashamba, kwa ajili yangu, atapokea mara mia zaidi, na kupata uzima wa milele.p
30Lakini walio wa kwanza watakuwa wa mwisho, na walio wa mwisho watakuwa wa kwanza.q