Hebrews 7:1-10
1Melkisedeki alikuwa mfalme wa Salemu, na kuhani wa Mungu Mkuu. Abrahamu alipokuwa anarudi kutoka vitani ambako aliwaua wafalme, Melkisedeki alikutana naye akambariki,
2naye Abrahamu akampa sehemu ya kumi ya vitu vyote alivyokuwa navyo. (Maana ya kwanza ya jina hili Melkisedeki ni “Mfalme wa Uadilifu”; na, kwa vile yeye alikuwa mfalme wa Salemu, jina lake pia lina maana ya “Mfalme wa Amani.”)
3Baba yake na mama yake hawatajwi, wala ukoo wake hautajwi; haisemwi alizaliwa lini au alikufa lini. Anafanana na Mwana wa Mungu, na anaendelea kuwa kuhani daima.
4Basi, mwaona jinsi mtu huyu alivyokuwa maarufu. Baba Abrahamu alimpa sehemu moja ya kumi ya vitu vyote alivyoteka vitani.
5Tunajua vilevile kwamba kufuatana na Sheria, wana wa Lawi ambao ni makuhani, wanayo haki ya kuchukua sehemu ya kumi kutoka kwa watu, yaani ndugu zao, ingawaje nao ni watoto wa Abrahamu.
6Lakini huyo Melkisedeki hakuwa wa ukoo wa Lawi, hata hivyo alipokea sehemu ya kumi kutoka kwa Abrahamu; tena akambariki yeye ambaye alikuwa amepewa ahadi ya Mungu.
7Hakuna mashaka hata kidogo kwamba anayebariki ni mkuu zaidi kuliko yule anayebarikiwa.
8Tena, hao makuhani wanaopokea sehemu ya kumi, ni watu ambao hufa; lakini hapa anayepokea sehemu ya kumi, yaani Melkisedeki, anasemekana kwamba hafi.
9Twaweza, basi, kusema kwamba Abrahamu alipotoa sehemu moja ya kumi, Lawi (ambaye watoto wake hupokea sehemu moja ya kumi) alitoa sehemu moja ya kumi pia.
10Maana Lawi hakuwa amezaliwa bado, bali ni kama alikuwa katika mwili wa baba yake, Abrahamu, wakati Melkisedeki alipokutana naye.